Amosi Mlango 4 Amos

Amosi 4:1

Lisikieni neno hili, enyi ng'ombe wa Bashani, mnaokaa juu ya mlima wa Samaria, mnaowaonea maskini, na kuwaponda wahitaji; mnaowaambia bwana zao, Haya! Leteni, tunywe.

Amosi 4:2

Bwana MUNGU ameapa kwa utakatifu wake, ya kuwa, tazama, siku zitawajilia, watakapowaondoa ninyi kwa kulabu, na mabaki yenu kwa ndoana.

Amosi 4:3

Nanyi mtatoka kwenye mahali palipobomolewa, kila mwanamke moja kwa moja mbele yake; nanyi mtajitupa katika Harmoni, asema Bwana.

Amosi 4:4

Njoni Betheli, mkakose; njoni Gilgali, mkaongeze makosa; kaleteni dhabihu zenu kila asubuhi, na zaka zenu kila siku ya tatu;

Amosi 4:5

mkachome sadaka ya shukrani, ya kitu kilichotiwa chachu; mkatangaze sadaka mtoazo kwa hiari na kuzihubiri habari zake; kwa maana ndivyo viwapendezavyo ninyi, enyi wana wa Israeli, asema Bwana MUNGU.

Amosi 4:6

Mimi nami nimewapa usafi wa meno katika miji yenu yote, na kutindikiwa na mkate mahali penu pote; lakini hamkunirudia mimi, asema Bwana.

Amosi 4:7

Tena nimeizuia mvua msiipate, ilipobaki miezi mitatu kabla ya mavuno; nami nimenyesha mvua juu ya mji mmoja, nikaizuia mvua isinyeshe juu ya mji mwingine; sehemu moja ilipata mvua, na sehemu isiyopata mvua ilikatika.

Amosi 4:8

Basi kutoka miji miwili mitatu walitanga-tanga kuendea mji mwingine wapate kunywa maji, wasipate ya kuwatosha; lakini hamkunirudia mimi, asema Bwana.

Amosi 4:9

Nami nimewapiga kwa ukavu na koga; wingi wa bustani zenu na mashamba yenu ya mizabibu, na mitini yenu na mizeituni yenu imeliwa na tunutu; Lakini hamkunirudia mimi, asema Bwana.

Amosi 4:10

Nimewapelekea tauni, kama tauni ya Misri; vijana wenu nimewaua kwa upanga, na farasi wenu nimewachukulia mbali; nami nimeupandisha uvundo wa matuo yenu na kuuingiza katika mianzi ya pua zenu; lakini hamkunirudia mimi, asema Bwana.

Amosi 4:11

Baadhi yenu nimewaangamiza, kama hapo Mungu alipoiangamiza Sodoma na Gomora, nanyi mkawa kama kinga kilichonyakuliwa motoni; lakini hamkunirudia mimi, asema Bwana.

Amosi 4:12

Basi nitakutenda hivi, Ee Israeli, na kwa sababu nitakutenda hivi, ujiweke tayari kuonana na Mungu wako, Ee Israeli.

Amosi 4:13

Kwa maana, angalia, yeye aifanyizaye milima, na kuuumba upepo, na kumwambia mwanadamu mawazo yake, afanyaye asubuhi kuwa giza, na kupakanyaga mahali pa dunia palipoinuka; Bwana, Mungu wa majeshi, ndilo jina lake.