Wafilipi Mlango 2 Philippians

Wafilipi 2:1

Basi ikiwako faraja yo yote katika Kristo, yakiwako matulizo yo yote ya mapenzi, ukiwako ushirika wo wote wa Roho, ikiwako huruma yo yote na rehema,

Wafilipi 2:2

ijalizeni furaha yangu, ili mwe na nia moja, wenye mapenzi mamoja, wenye roho moja, mkinia mamoja.

Wafilipi 2:3

Msitende neno lo lote kwa kushindana wala kwa majivuno; bali kwa unyenyekevu, kila mtu na amhesabu mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi yake.

Wafilipi 2:4

Kila mtu asiangalie mambo yake mwenyewe, bali kila mtu aangalie mambo ya wengine.

Wafilipi 2:5

Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu;

Wafilipi 2:6

ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho;

Wafilipi 2:7

bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu;

Wafilipi 2:8

tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba.

Wafilipi 2:9

Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina;

Wafilipi 2:10

ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi;

Wafilipi 2:11

na kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI Bwana, kwa utukufu wa Mungu Baba.

Wafilipi 2:12

Basi, wapendwa wangu, kama vile mlivyotii sikuzote, si wakati mimi nilipokuwapo tu, bali sasa zaidi sana mimi nisipokuwapo, utimizeni wokovu wenu wenyewe kwa kuogopa na kutetemeka.

Wafilipi 2:13

Kwa maana ndiye Mungu atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu, kwa kulitimiza kusudi lake jema.

Wafilipi 2:14

Yatendeni mambo yote pasipo manung'uniko wala mashindano,

Wafilipi 2:15

mpate kuwa wana wa Mungu wasio na lawama, wala udanganyifu, wasio na ila kati ya kizazi chenye ukaidi, kilichopotoka; ambao kati ya hao mnaonekana kuwa kama mianga katika ulimwengu,

Wafilipi 2:16

mkishika neno la uzima; nipate sababu ya kuona fahari katika siku ya Kristo, ya kuwa sikupiga mbio bure wala sikujitaabisha bure.

Wafilipi 2:17

Naam, hata nikimiminwa juu ya dhabihu na ibada ya imani yenu, nafurahi; tena nafurahi pamoja nanyi nyote.

Wafilipi 2:18

Nanyi vivyo hivyo furahini, tena furahini pamoja nami.

Wafilipi 2:19

Walakini natumaini katika Bwana Yesu kumtuma Timotheo afike kwenu karibu, nifarijiwe na mimi, nikiijua hali yenu.

Wafilipi 2:20

Maana sina mtu mwingine mwenye nia moja nami, atakayeiangalia hali yenu kweli kweli.

Wafilipi 2:21

Maana wote wanatafuta vyao wenyewe, sivyo vya Kristo Yesu.

Wafilipi 2:22

Ila mwajua sifa yake, ya kuwa ametumika pamoja nami kwa ajili ya Injili, kama mwana na baba yake.

Wafilipi 2:23

Basi, natumaini kumtuma huyo mara, hapo nitakapojua yatakayonipata.

Wafilipi 2:24

Nami naamini katika Bwana ya kuwa nitakuja na mimi mwenyewe hivi karibu.

Wafilipi 2:25

Lakini naliona imenilazimu kumtuma kwenu Epafrodito, ndugu yangu, mtenda kazi pamoja nami, askari pamoja nami; tena ni mtume wenu na mhudumu wa mahitaji yangu.

Wafilipi 2:26

Kwa kuwa alikuwa na shauku kwenu ninyi nyote, akahuzunika sana, kwa sababu mlisikia ya kwamba alikuwa hawezi.

Wafilipi 2:27

Kwa maana alikuwa hawezi kweli kweli, karibu na kufa; lakini Mungu alimhurumia; wala si yeye peke yake, ila na mimi pia; nisiwe na huzuni juu ya huzuni.

Wafilipi 2:28

Kwa hiyo nimefanya bidii nyingi zaidi kumtuma, ili mtakapomwona tena mpate kufurahi, nami nipunguziwe huzuni yangu.

Wafilipi 2:29

Mpokeeni, basi, katika Bwana, kwa furaha yote, mkawahesabu watu kama huyu kuwa watu wa kuheshimiwa.

Wafilipi 2:30

Maana kwa ajili ya kazi ya Kristo alikaribia kufa akaponza roho yake; ili kusudi ayatimize yaliyopungua katika huduma yenu kwangu.