Mika Mlango 5 Micah

Mika 5:1

Sasa utajikusanya vikosi vikosi, Ee binti wa vikosi; yeye amemhusuru; watampiga mwamuzi wa Israeli shavuni mwake kwa fimbo.

Mika 5:2

Bali wewe, Bethlehemu Efrata, uliye mdogo kuwa miongoni mwa elfu za Yuda; kutoka kwako wewe atanitokea mmoja atakayekuwa mtawala katika Israeli; ambaye matokeo yake yamekuwa tangu zamani za kale, tangu milele.

Mika 5:3

Kwa sababu hiyo atawatoa, hata wakati wa kuzaa kwake aliye na utungu; ndipo hayo mabaki ya nduguze watawarudia wana wa Israeli.

Mika 5:4

Naye atasimama, na kulisha kundi lake kwa nguvu za Bwana, kwa enzi ya jina la Bwana, Mungu wake; nao watakaa; maana sasa atakuwa mkuu hata miisho ya dunia.

Mika 5:5

Na mtu huyu atakuwa amani yetu; wakati Mwashuri atakapoingia katika nchi yetu, na kuyakanyaga majumba yetu, hapo mtaondokesha wachungaji saba juu yake, na wakuu wanane.

Mika 5:6

Nao wataiharibu nchi ya Ashuru kwa upanga, na nchi ya Nimrodi katika malango yake; naye atatuokoa na Mwashuri, atakapoingia katika nchi yetu, na kukanyaga ndani ya mipaka yetu.

Mika 5:7

Na hayo mabaki ya Yakobo yatakuwa kati ya kabila nyingi mfano wa umande utokao kwa Bwana, mfano wa manyunyu katika manyasi; yasiyomngojea mtu, wala kuwakawilia wanadamu.

Mika 5:8

Na hayo mabaki ya Yakobo yatakuwa kati ya mataifa, kati ya kabila nyingi, mfano wa simba kati ya wanyama wa msituni, kama mwana-simba kati ya makundi ya kondoo, ambaye, akiwa anapita katikati, hukanyaga-kanyaga na kurarua-rarua, wala hakuna wa kuokoa.

Mika 5:9

Mkono wako na uinuliwe juu ya adui zako, na adui zako wote wakauliwe mbali.

Mika 5:10

Kisha itakuwa katika siku hiyo, asema Bwana, nitawakatilia mbali farasi zako watoke kati yako, nami nitayaharibu magari yako ya vita;

Mika 5:11

nami nitaikatilia mbali miji ya nchi yako, na ngome zako zote nitaziangusha;

Mika 5:12

nami nitakatilia mbali uchawi, usiwe mkononi mwako; wala hutakuwa tena na watu wenye kutabana;

Mika 5:13

nami nitakatilia mbali sanamu zako na nguzo zako, zitoke kati yako; wala hutaiabudu tena kazi ya mikono yako.

Mika 5:14

Nami nitayang'oa maashera yenu, yasiwe kati yako; nami nitaiangamiza miji yako.

Mika 5:15

Nami nitajilipiza kisasi katika hasira na ghadhabu juu ya mataifa wasiosikiliza.