Mika Mlango 4 Micah

Mika 4:1

Lakini itakuwa katika siku za mwisho, ya kwamba mlima wa nyumba ya Bwana utawekwa imara juu ya milima, nao utainuliwa juu ya vilima; na watu wa mataifa watauendea makundi makundi.

Mika 4:2

Na mataifa mengi watakwenda na kusema, Njoni, twende juu mlimani kwa Bwana, na nyumbani kwa Mungu wa Yakobo; naye atatufundisha njia zake, nasi tutakwenda katika mapito yake; kwa maana katika Sayuni itatoka sheria, na neno la Bwana litatoka Yerusalemu.

Mika 4:3

Naye atafanya hukumu kati ya watu wa kabila nyingi, naye atawakemea mataifa wenye nguvu walio mbali; nao watafua panga zao ziwe majembe, na mikuki yao iwe miundu; taifa halitainua upanga juu ya taifa lingine, wala hawatajifunza vita tena kamwe.

Mika 4:4

Bali wataketi kila mtu chini ya mzabibu wake, na chini ya mtini wake; wala hapana mtu atakayewatia hofu; kwa kuwa kinywa cha Bwana wa majeshi kimesema hivi.

Mika 4:5

Kwa maana mataifa yote watakwenda, kila moja kwa jina la mungu wake, na sisi tutakwenda kwa jina la Bwana, Mungu wetu, milele na milele.

Mika 4:6

Katika siku ile, asema Bwana, nitamkusanya yeye achechemeaye, nami nitamrudisha yeye aliyefukuzwa, na yeye niliyemtesa.

Mika 4:7

Nami nitamfanya yeye aliyechechemea kuwa mabaki, na yeye aliyetupwa mbali kuwa taifa lenye nguvu, na Bwana atawamiliki katika mlima Sayuni tangu sasa na hata milele.

Mika 4:8

Na wewe, Ee mnara wa kundi, kilima cha binti Sayuni, utajiliwa; naam, mamlaka ya kwanza yatakuja, ufalme wa binti Yerusalemu.

Mika 4:9

Sasa mbona unapiga kelele? Je! Hakuna mfalme kwako, mshauri wako amepotea, hata umeshikwa na utungu kama mwanamke wakati wa kuzaa?

Mika 4:10

Uwe na utungu, utaabike ili uzae, Ee binti Sayuni, kama mwanamke mwenye utungu; maana sasa utatoka mjini, nawe utakaa katika mashamba; utafika hata Babeli; huko ndiko utakakookolewa; huko ndiko Bwana atakakokukomboa katika mikono ya adui zako.

Mika 4:11

Na sasa mataifa mengi wamekusanyika juu yako, wasemao, Na atiwe unajisi; macho yetu na yaone shari ya Sayuni.

Mika 4:12

Lakini wao hawayajui mawazo ya Bwana, wala hawafahamu shauri lake; kwa maana amewakusanya kama miganda sakafuni.

Mika 4:13

Haya, simama upure, Ee binti Sayuni; kwa maana nitafanya pembe yako kuwa chuma, na kwato zako kuwa shaba; nawe utaponda-ponda mataifa mengi, na faida yao utaiweka wakfu kwa Bwana, na mali zao kwa Bwana wa dunia yote.