2 Petro Mlango 1 2nd Peter

2 Petro 1:1

Simoni Petro, mtumwa na mtume wa Yesu Kristo, kwa wale waliopata imani moja na sisi, yenye thamani, katika hali ya Mungu wetu, na Mwokozi Yesu Kristo.

2 Petro 1:2

Neema na iwe kwenu na amani iongezwe katika kumjua Mungu na Yesu Bwana wetu.

2 Petro 1:3

Kwa kuwa uweza wake wa Uungu umetukirimia vitu vyote vipasavyo uzima na utauwa, kwa kumjua yeye aliyetuita kwa utukufu wake na wema wake mwenyewe.

2 Petro 1:4

Tena kwa hayo ametukirimia ahadi kubwa mno, za thamani, ili kwamba kwa hizo mpate kuwa washirika wa tabia ya Uungu, mkiokolewa na uharibifu uliomo duniani kwa sababu ya tamaa.

2 Petro 1:5

Naam, na kwa sababu iyo hiyo mkijitahidi sana kwa upande wenu, katika imani yenu tieni na wema, na katika wema wenu maarifa,

2 Petro 1:6

na katika maarifa yenu kiasi, na katika kiasi chenu saburi, na katika saburi yenu utauwa,

2 Petro 1:7

na katika utauwa wenu upendano wa ndugu, na katika upendano wa ndugu, upendo.

2 Petro 1:8

Maana mambo hayo yakiwa kwenu na kujaa tele, yawafanya ninyi kuwa si wavivu wala si watu wasio na matunda, kwa kumjua Bwana wetu Yesu Kristo.

2 Petro 1:9

Maana yeye asiyekuwa na hayo ni kipofu, hawezi kuona vitu vilivyo mbali, amesahau kule kutakaswa dhambi zake za zamani.

2 Petro 1:10

Kwa hiyo ndugu, jitahidini zaidi kufanya imara kuitwa kwenu na uteule wenu; maana mkitenda hayo hamtajikwaa kamwe.

2 Petro 1:11

Maana hivi mtaruzukiwa kwa ukarimu kuingia katika ufalme wa milele wa Bwana wetu, Mwokozi wetu Yesu Kristo.

2 Petro 1:12

Kwa hiyo nitakuwa tayari kuwakumbusha hayo siku zote, ijapokuwa mnayajua na kuthibitishwa katika kweli mliyo nayo.

2 Petro 1:13

Nami naona ni haki, maadamu nipo mimi katika maskani hii, kuwaamsha kwa kuwakumbusha.

2 Petro 1:14

Nikijua kwamba kule kuwekea mbali maskani yangu kwaja upesi, kama Bwana wetu Yesu Kristo alivyonionyesha.

2 Petro 1:15

Walakini nitajitahidi, kwamba kila wakati baada ya kufariki kwangu mpate kuyakumbuka mambo hayo.

2 Petro 1:16

Maana hatukufuata hadithi zilizotungwa kwa werevu, tulipowajulisha ninyi nguvu zake Bwana wetu Yesu Kristo na kuja kwake; bali tulikuwa tumeuona wenyewe ukuu wake.

2 Petro 1:17

Maana alipata kwa Mungu Baba heshima na utukufu, hapo alipoletewa sauti iliyotoka katika utukufu mkuu, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye.

2 Petro 1:18

Na sauti hiyo sisi tuliisikia ikitoka mbinguni tulipokuwa pamoja naye katika mlima ule mtakatifu.

2 Petro 1:19

Nasi tuna lile neno la unabii lililo imara zaidi, ambalo, mkiliangalia, kama taa ing'aayo mahali penye giza, mwafanya vyema, mpaka kutakapopambazuka, na nyota ya asubuhi kuzuka mioyoni mwenu.

2 Petro 1:20

Mkijua neno hili kwanza, ya kwamba hakuna unabii katika maandiko upatao kufasiriwa kama apendavyo mtu fulani tu.

2 Petro 1:21

Maana unabii haukuletwa po pote kwa mapenzi ya mwanadamu; bali wanadamu walinena yaliyotoka kwa Mungu, wakiongozwa na Roho Mtakatifu.