3 Yohana Mlango 1 3rd John

3 Yohana 1:1

Mzee, kwa Gayo mpenzi, nimpendaye katika kweli.

3 Yohana 1:2

Mpenzi naomba ufanikiwe katika mambo yote na kuwa na afya yako, kama vile roho yako ifanikiwavyo.

3 Yohana 1:3

Maana nalifurahi mno walipokuja ndugu na kuishuhudia kweli yako, kama uendavyo katika kweli.

3 Yohana 1:4

Sina furaha iliyo kuu kuliko hii, kusikia ya kwamba watoto wangu wanakwenda katika kweli.

3 Yohana 1:5

Mpenzi, kazi ile ni ya uaminifu uwatendeayo hao ndugu na hao wageni nao,

3 Yohana 1:6

waliokushuhudia upendo wako mbele ya kanisa; utafanya vizuri ukiwasafirisha kama ipasavyo kwa Mungu.

3 Yohana 1:7

Kwa maana, kwa ajili ya Jina hilo, walitoka, wasipokee kitu kwa Mataifa.

3 Yohana 1:8

Basi imetupasa sisi kuwakaribisha watu kama hao, ili tuwe watenda kazi pamoja na kweli.

3 Yohana 1:9

Naliliandikia kanisa neno, lakini Diotrefe, apendaye kuwa wa kwanza kati yao, hatukubali.

3 Yohana 1:10

Kwa hiyo, nikija, nitayakumbuka matendo yake atendayo, atoavyo upuzi juu yetu kwa maneno maovu; wala hatoshwi na hayo, ila yeye mwenyewe hawakaribishi hao ndugu, na wale watakao kuwakaribisha, huwazuia, na kuwatoa katika kanisa.

3 Yohana 1:11

Mpenzi, usiuige ubaya, bali uige wema. Yeye atendaye mema ni wa Mungu, bali yeye atendaye mabaya hakumwona Mungu.

3 Yohana 1:12

Demetrio ameshuhudiwa na watu wote, tena na ile kweli yenyewe. Nasi pia twashuhudia, nawe wajua ya kwamba ushuhuda wetu ni kweli.

3 Yohana 1:13

Nalikuwa na mambo mengi ya kukuandikia, lakini sipendi kukuandikia kwa wino na kalamu.

3 Yohana 1:14

Lakini nataraji kukuona karibu, nasi tutasema uso kwa uso.