Ufunuo wa Yohana Mlango 2 Revelation

Ufunuo wa Yohana 2:1

Kwa malaika wa kanisa lililoko Efeso andika; Haya ndiyo anenayo yeye azishikaye hizo nyota saba katika mkono wake wa kuume, yeye aendaye katikati ya vile vinara saba vya dhahabu.

Ufunuo wa Yohana 2:2

Nayajua matendo yako, na taabu yako, na subira yako, na ya kuwa huwezi kuchukuliana na watu wabaya, tena umewajaribu wale wajiitao mitume, nao sio, ukawaona kuwa waongo;

Ufunuo wa Yohana 2:3

tena ulikuwa na subira na kuvumilia kwa ajili ya jina langu, wala hukuchoka.

Ufunuo wa Yohana 2:4

Lakini nina neno juu yako, ya kwamba umeuacha upendo wako wa kwanza.

Ufunuo wa Yohana 2:5

Basi, kumbuka ni wapi ulikoanguka; ukatubu, ukayafanye matendo ya kwanza. Lakini, usipofanya hivyo, naja kwako, nami nitakiondoa kinara chako katika mahali pake, usipotubu.

Ufunuo wa Yohana 2:6

Lakini unalo neno hili, kwamba wayachukia matendo ya Wanikolai, ambayo na mimi nayachukia.

Ufunuo wa Yohana 2:7

Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa. Yeye ashindaye, nitampa kula matunda ya mti wa uzima, ulio katika bustani ya Mungu.

Ufunuo wa Yohana 2:8

Na kwa malaika wa kanisa lililoko Smirna andika; Haya ndiyo aneneyo yeye aliye wa kwanza na wa mwisho, aliyekuwa amekufa, kisha akawa hai.

Ufunuo wa Yohana 2:9

Naijua dhiki yako na umaskini wako, (lakini u tajiri) najua na matukano ya hao wasemao ya kuwa ni Wayahudi, nao sio, bali ni sinagogi la Shetani.

Ufunuo wa Yohana 2:10

Usiogope mambo yatakayokupata; tazama, huyo Ibilisi atawatupa baadhi yenu gerezani ili mjaribiwe, nanyi mtakuwa na dhiki siku kumi. Uwe mwaminifu hata kufa, nami nitakupa taji ya uzima.

Ufunuo wa Yohana 2:11

Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa. Yeye ashindaye hatapatikana na madhara ya mauti ya pili.

Ufunuo wa Yohana 2:12

Na kwa malaika wa kanisa lililoko Pergamo andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye na huo upanga mkali, wenye makali kuwili.

Ufunuo wa Yohana 2:13

Napajua ukaapo, ndipo penye kiti cha enzi cha Shetani; nawe walishika sana jina langu, wala hukuikana imani yangu, hata katika siku za Antipa shahidi wangu, mwaminifu wangu, aliyeuawa kati yenu, hapo akaapo Shetani.

Ufunuo wa Yohana 2:14

Lakini ninayo maneno machache juu yako, kwa kuwa unao huko watu washikao mafundisho ya Balaamu, yeye aliyemfundisha Balaki atie ukwazo mbele ya Waisraeli, kwamba wavile vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na kuzini.

Ufunuo wa Yohana 2:15

Vivyo hivyo wewe nawe unao watu wayashikao mafundisho ya Wanikolai vile vile.

Ufunuo wa Yohana 2:16

Basi tubu; na usipotubu, naja kwako upesi, nami nitafanya vita juu yao kwa huo upanga wa kinywa changu.

Ufunuo wa Yohana 2:17

Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa. Yeye ashindaye nitampa baadhi ya ile mana iliyofichwa, nami nitampa jiwe jeupe, na juu ya jiwe hilo limeandikwa jina jipya asilolijua mtu ila yeye anayelipokea.

Ufunuo wa Yohana 2:18

Na kwa malaika wa kanisa lililoko Thiatira andika; Haya ndiyo anenayo Mwana wa Mungu, yeye aliye na macho yake kama mwali wa moto, na miguu yake mfano wa shaba iliyosuguliwa sana.

Ufunuo wa Yohana 2:19

Nayajua matendo yako na upendo na imani na huduma na subira yako; tena kwamba matendo yako ya mwisho yamezidi yale ya kwanza.

Ufunuo wa Yohana 2:20

Lakini nina neno juu yako, ya kwamba wamridhia yule mwanamke Yezebeli, yeye ajiitaye nabii na kuwafundisha watumishi wangu na kuwapoteza, ili wazini na kula vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu.

Ufunuo wa Yohana 2:21

Nami nimempa muda ili atubu, wala hataki kuutubia uzinzi wake.

Ufunuo wa Yohana 2:22

Tazama, nitamtupa juu ya kitanda, na hao wazinio pamoja naye, wapate dhiki kubwa wasipotubia matendo yake;

Ufunuo wa Yohana 2:23

nami nitawaua watoto wake kwa mauti. Na makanisa yote watajua ya kuwa mimi ndiye achunguzaye viuno na mioyo. Nami nitampa kila mmoja wenu kwa kadiri ya matendo yake.

Ufunuo wa Yohana 2:24

Lakini nawaambia ninyi wengine mlioko Thiatira, wo wote wasio na mafundisho hayo, wasiozijua fumbo za Shetani, kama vile wasemavyo, Sitaweka juu yenu mzigo mwingine.

Ufunuo wa Yohana 2:25

Ila mlicho nacho kishikeni sana, hata nitakapokuja.

Ufunuo wa Yohana 2:26

Na yeye ashindaye, na kuyatunza matendo yangu hata mwisho, nitampa mamlaka juu ya mataifa,

Ufunuo wa Yohana 2:27

naye atawachunga kwa fimbo ya chuma, kama vyombo vya mfinyanzi vipondwavyo, kama mimi nami nilivyopokea kwa Baba yangu.

Ufunuo wa Yohana 2:28

Nami nitampa ile nyota ya asubuhi.

Ufunuo wa Yohana 2:29

Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa.