Ufunuo wa Yohana Mlango 10 Revelation

Ufunuo wa Yohana 10:1

Kisha nikaona malaika mwingine mwenye nguvu akishuka kutoka mbinguni, amevikwa wingu; na upinde wa mvua juu ya kichwa chake; na uso wake ulikuwa kama jua, na miguu yake kama nguzo za moto.

Ufunuo wa Yohana 10:2

Na katika mkono wake alikuwa na kitabu kidogo kimefunguliwa. Akaweka mguu wake wa kuume juu ya bahari, nao wa kushoto juu ya nchi.

Ufunuo wa Yohana 10:3

Naye akalia kwa sauti kuu, kama simba angurumavyo. Na alipolia, zile ngurumo saba zikatoa sauti zao.

Ufunuo wa Yohana 10:4

Hata ngurumo saba zilipotoa sauti zao, nalikuwa tayari kuandika. Nami nalisikia sauti kutoka mbinguni ikisema, Yatie muhuri maneno hayo yaliyonenwa na hizo ngurumo saba, usiyaandike.

Ufunuo wa Yohana 10:5

Na yule malaika niliyemwona, akisimama juu ya bahari na juu ya nchi, akainua mkono wake wa kuume kuelekea mbinguni,

Ufunuo wa Yohana 10:6

akaapa kwa yeye aliye hai hata milele na milele, yeye aliyeziumba mbingu na vitu vilivyomo, na nchi na vitu vilivyomo, na bahari na vitu vilivyomo, ya kwamba hapatakuwa na wakati baada ya haya;

Ufunuo wa Yohana 10:7

isipokuwa katika siku za sauti ya malaika wa saba atakapokuwa tayari kupiga baragumu; hapo ndipo siri ya Mungu itakapotimizwa, kama alivyowahubiri watumishi wake hao manabii.

Ufunuo wa Yohana 10:8

Na sauti ile niliyoisikia kutoka mbinguni ilinena nami tena, ikisema, Enenda, ukakitwae kile kitabu kilichofunguliwa katika mkono wa yule malaika, aliyesimama juu ya bahari na juu ya nchi.

Ufunuo wa Yohana 10:9

Nikamwendea malaika yule nikamwambia kwamba anipe kile kitabu kidogo. Akaniambia, Kitwae, ukile, nacho kitakutia uchungu tumboni mwako, bali katika kinywa chako kitakuwa kitamu kama asali.

Ufunuo wa Yohana 10:10

Nikakitwaa kile kitabu kidogo katika mkono wa malaika yule, nikakila; nacho kikawa kitamu kama asali kinywani mwangu, na nilipokwisha kukila tumbo langu likatiwa uchungu.

Ufunuo wa Yohana 10:11

Wakaniambia, Imekupasa kutoa unabii tena juu ya watu na taifa na lugha na wafalme wengi.