Ufunuo wa Yohana Mlango 17 Revelation

Ufunuo wa Yohana 17:1

Akaja mmoja wa wale malaika saba, wenye vile vitasa saba, akanena nami, akisema, Njoo huku, nitakuonyesha hukumu ya yule kahaba mkuu aketiye juu ya maji mengi;

Ufunuo wa Yohana 17:2

ambaye wafalme wa nchi wamezini naye, nao wakaao katika nchi wamelevywa kwa mvinyo ya uasherati wake.

Ufunuo wa Yohana 17:3

Akanichukua katika Roho hata jangwani, nikaona mwanamke, ameketi juu ya mnyama mwekundu sana, mwenye kujaa majina ya makufuru, mwenye vichwa saba na pembe kumi.

Ufunuo wa Yohana 17:4

Na mwanamke yule alikuwa amevikwa nguo ya rangi ya zambarau, na nyekundu, amepambwa kwa dhahabu, na kito cha thamani, na lulu, naye alikuwa na kikombe cha dhahabu mkononi mwake, kilichojawa na machukizo, na machafu ya uasherati wake.

Ufunuo wa Yohana 17:5

Na katika kipaji cha uso wake alikuwa na jina limeandikwa, la siri, BABELI MKUU, MAMA WA MAKAHABA NA MACHUKIZO YA NCHI.

Ufunuo wa Yohana 17:6

Nikamwona yule mwanamke amelewa kwa damu ya watakatifu, na kwa damu ya mashahidi wa Yesu. Nami nilipomwona nikastaajabu ajabu kuu.

Ufunuo wa Yohana 17:7

Na yule malaika akaniambia, Kwani kustaajabu? Nitakuambia siri ya mwanamke huyu, na ya mnyama huyu amchukuaye, mwenye vile vichwa saba na zile pembe kumi.

Ufunuo wa Yohana 17:8

Yule mnyama uliyemwona alikuwako, naye hayuko, naye yu tayari kupanda kutoka kuzimu na kwenda kwenye uharibifu. Na hao wakaao juu ya nchi, wasioandikwa majina yao katika kitabu cha uzima tangu kuwekwa misingi ya ulimwengu, watastaajabu wamwonapo yule mnyama, ya kwamba alikuwako, naye hayuko, naye atakuwako.

Ufunuo wa Yohana 17:9

Hapo ndipo penye akili zenye hekima. Vile vichwa saba ni milima saba anayokalia mwanamke huyo.

Ufunuo wa Yohana 17:10

Navyo ni wafalme saba. Watano wamekwisha kuanguka, na mmoja yupo, na mwingine hajaja bado. Naye atakapokuja imempasa kukaa muda mchache.

Ufunuo wa Yohana 17:11

Na yule mnyama aliyekuwako naye hayuko, yeye ndiye wa nane, naye ni mmoja wa wale saba, naye aenenda kwenye uharibifu.

Ufunuo wa Yohana 17:12

Na zile pembe kumi ulizoziona ni wafalme kumi, ambao hawajapokea ufalme bado, lakini wapokea mamlaka kama wafalme muda wa saa moja pamoja na yule mnyama.

Ufunuo wa Yohana 17:13

Hawa wana shauri moja, nao wampa yule mnyama nguvu zao na mamlaka yao.

Ufunuo wa Yohana 17:14

Hawa watafanya vita na Mwana-Kondoo, na Mwana Kondoo atawashinda, kwa maana Yeye ni Bwana wa Mabwana, na Mfalme wa Wafalme, na hao walio pamoja naye ndio walioitwa, na wateule, na waaminifu.

Ufunuo wa Yohana 17:15

Kisha akaniambia, Yale maji uliyoyaona, hapo aketipo yule kahaba, ni jamaa na makutano na mataifa na lugha.

Ufunuo wa Yohana 17:16

Na zile pembe kumi ulizoziona, na huyo mnyama, hao watamchukia yule kahaba, nao watamfanya kuwa mkiwa na uchi, watamla nyama yake, watamteketeza kabisa kwa moto.

Ufunuo wa Yohana 17:17

Maana Mungu ametia mioyoni mwao kufanya shauri lake, na kufanya shauri moja, na kumpa yule mnyama ufalme wao hata maneno ya Mungu yatimizwe.

Ufunuo wa Yohana 17:18

Na yule mwanamke uliyemwona, ni mji ule mkubwa, wenye ufalme juu ya wafalme wa nchi.